2 Wathesalonike 3 (Swahili SRB 37)
1Kisha, ndugu, mtuombee sisi kwa Mungu, Neno la Bwana liendelee na kutukuzwa vivyo hivyo kama kwenu! 2Tena tuombeeni, tuokolewe mikononi mwa watu walio wapuzi na wabaya! Kwani sio wote wawezao kumtegemea Bwana. 3Lakini Bwana ni mwelekevu atakayewashupaza na kuwalinda, yule Mbaya asiwajie. 4Kwa ajili yenu tunamtumaini Bwana kwamba: Tunayowaagiza, mwayashika sasa, hata siku za nyuma mtayashika. 5Bwana aiongoze mioyo yenu, iufikie upendo wa Mungu na uvumilivu wa Kristo! 6*Ndugu, tunawaagiza ninyi, kwa nguvu ya Jina la Bwana Yesu Kristo, mtengane na kila ndugu anayeendelea na kufuata mambo yaliyo ya ovyoovyo tu, asiufuate ufundisho, mlioupata kwetu sisi. 7Kwani mwajua wenyewe, jinsi inavyowapasa kutuiga, kwa sababu hatukukaa kwenu kiovyoovyo tu. 8Hakuna, ambaye tulikula chakula chake bure, ila tulijisumbua na kujiumiza tukifanya kazi usiku na mchana kwa kukataa kumlemea mtu ye yote wa kwenu. 9Hatukuvifanya hivyo kwamba: Hatu wakuu, ila tulitaka kuwapa ninyi vielezo, mpate kutuiga. 10Kwani tulipokuwa kwenu tuliwaagiza hata neno hili: Mtu asiyetaka kufanya kazi asipate chakula! 11Kwani twasikia: Kwenu wako wanaoendelea na kufuata mambo yaliyo ya ovyoovyo tu, hawafanyi kazi, ila hufanya mapuzi. 12Walio hivyo tunawaagiza na kuwaonya machoni pake Bwana Yesu Kristo, watulie, wapate kufanya kazi na kula chakula chao wenyewe. 13Lakini ninyi, ndugu, msichoke kufanya yaliyo mazuri!* 14Lakini mtu asipoyatii maneno yetu yaliyomo humu baruani, huyo mjulisheni mkikataa kuchanganika naye, apatwe na soni! 15Lakini msimwazie kuwa mchukivu, ila mwonyeni kindugu! 16Lakini yeye Bwana aliye mwenye utangemano awape kutengemana po pote katika mambo yote! Bwana awe nanyi nyote! 17Salamu hii naiandika kwa mkono wangu mimi Paulo; huu ndio mwandiko wangu katika barua zote. Hivi ndivyo, ninavyoandika. 18Upole wa Bwana wetu Yesu Kristo uwakalie ninyi nyote! Amin.

