Waefeso 2 (Swahili SRB 37)
1Nanyi mlikuwa mmekufa kwa ajili ya maanguko na makosa yenu, 2mliyoendelea nayo kale kwa desturi za watu walio wa ulimwengu huu tu; ndivyo, mwenye kuzitawala nguvu za angani atakavyo, ni yule pepo anayetenda nguvu hata sasa mwao waliokataa kutii. 3Nasi sote kale tulikuwa wenzao tulipoendelea na kuzifuata tamaa za miili yetu na kuyafanya, miili na mioyo yetu iliyoyataka, nasi kwa hivyo, tulivyokuwa hapo, tulikuwa wana waliomkasirisha kama wale wengine. 4*Lakini Mungu alikuwa ametulimbikia huruma kwa kuwa na upendo mwingi wa kutupenda; 5kwa sababu hiyo akaturudisha uzimani pamoja na Kristo hapo, tulipokuwa tumekufa kwa ajili ya maanguko; hivyo wokovu wenu ni gawio tu. 6Alipokwisha kutufufua pamoja naye akatukalisha mbinguni pake Kristo Yesu. 7Maana siku zitakazokuja anataka kuonyesha, magawio yake yanavyokuwa mengi, yasipimike akituendea kwa utu tu katika Kristo Yesu. 8Kwani wokovu wenu ni gawio tu, mlilopewa kwa ajili ya kumtegemea, nako hakukutoka mwenu, maana nako ni kipaji chake Mungu, 9nacho hamkukipata kwa kazi zenu, mtu asipate kujivuna. 10Kwani sisi tu kazi yake yeye, namo mwake Kristo Yesu ndimo, tulimoumbiwa, tufanye matendo mema, Mungu aliyotutengenezea kale, tuyafuate.* 11Kwa hiyo yakumbukeni: kale mlikuwa wamizimu kwa hivyo, miili yenu ilivyo; mkaitwa mapumbavu nao wale waliojiita makungwi, kwa sababu walikuwa wametahiriwa na mikono ya watu miilini mwao. 12Kumbukeni: siku zile mlikuwa hamnaye Kristo, tena mlikuwa mmekatazwa kuwa wenyeji kwao Waisiraeli, mkawa wageni, msiyajue maagano, waliyoagiwa kuyapata. Mlikuwa hamnacho kingojeo, wala hamnaye Mungu huku ulimwenguni. 13Lakini sasa kwa kuwa wake Kristo Yesu nanyi mliokuwa kale mbali mmeletwa na damu ya Kristo, mfike karibu. 14Kwani yeye ni utengemano wetu, maana yale makundi mawili aliyageuza kuwa moja, akiuvunja ukingo uliotutenga, tuchukizane. 15Ilikuwa hapo, alipoyatangua mwilini mwake yale maonyo na maagizo yaliyokuwa ya miiko tu. Akataka kuwaumba hao wote wawili kuwa mtu mmoja mpya aliye wake yeye; kwa hiyo aliwapatanisha, 16akawa kole yao wote wawili alipomlipa Mungu madeni yao yeye mmoja mwilini mwake, alipowambwa msalabani; huko ndiko, alikoyaua yale machukivu. 17Kisha akaja kuipiga hiyo mbiu njema ya utengemano kwenu ninyi mliokuwa mbali, nako kwao waliokuwa karibu. 18Kwani kwake yeye sote wawili tumepata njia ya kumfikia Baba, tukiwa wenye Roho moja. 19*Kwa hiyo sasa ham wageni tena, wala wenye kukaa kando, ila m wenyeji pamoja nao watakatifu, tena m wa nyumbani mwake Mungu. 20Mmejengwa juu ya msingi wao mitume na wafumbuaji, ambao Kristo Yesu ni jiwe lake la pembeni. 21Kwa nguvu yake yeye jengo lote linaunganishwa, lipate kukua, mpaka liwe nyumba takatifu, Bwana alimo. 22Humu nanyi mnajengwa pamoja na wengine, mwe kao lake Mungu la Kiroho.*

