Isaya 4 (Swahili SRB 37)
1Siku ile wake saba watamshika mume mmoja na kumwambia: Tutajipatia wenyewe vilaji na mavazi, tunataka tu kuitwa kwa jina lako, utuondolee soni zetu! 2Siku ile mche wa Bwana utakuwa wenye urembo na macheo, nao uzao wa nchi utakuwa wenye ukuu na utukufu kwao Waisiraeli waliopona. 3Atakayekuwa amebakizwa Sioni, naye atakayekuwa amesazwa Yerusalemu ataitwa mtakatifu, ni kila mmoja wao aliyeandikiwa kuwapo Yerusalemu. 4Hapo ndipo, Bwana atakapokuwa amekwisha kuyaosha machafu yao wanawali wa Sioni, napo ndipo, atakapokuwa amekwisha kuzitowesha mwao damu zilizomwagwa Yerusalemu; atavifanya kwa nguvu za roho yenye mapatilizo na kwa nguvu za roho yenye moto. 5Kwenye makao yote ya mlimani kwa Sioni nako kwenye makutano ya kumtambikia Bwana atakuumbia siku zote wingu litakalokuwa lenye moshi la mchana na lenye mwanga wa moto uwakao usiku, kwani chote chenye utukufu hupaswa na kifuniko chake. 6Hivyo watapata pa kukalia kivulini mchana, ukali wa jua usiwaumize, tena pa kukimbilia na pa kujifichia, kimbunga kisiwaangushe, wala mvua isiwapige.

