Zaburi 2 (Swahili SRB 37)
1Mbona wamizimu hupiga makelele? Mbona makabila ya watu huwaza mambo yaliyo ya bure? 2Wafalme wa nchi hushikana mioyo, wakuu nao hula njama wakikaa pamoja, wamkatae Bwana na Masiya wake kwamba: 3Na tuyavunje mafungo yao! na tuzitupe kamba zao, zisitufunge tena! 4Lakini akaaye mbinguni anawacheka, yeye Bwana anawafyoza. 5Siku zitakapotimia, atasema nao kwa makali yake, awastushe kwa moto wa machafuko yake: 6Mimi nimemsimika mfalme wangu huko mlimani kwa Sioni kwenye utukufu wangu. 7Nitasimulia shauri, Bwana aliloniambia: Wewe ndiwe Mwanangu, siku hii ya leo mimi nimekuzaa. 8Omba kwangu! Nami nitakupa wamizimu, wawe fungu lako, nayo mapeo ya nchi, yawe mali zako! 9Kwa fimbo ya chuma utawaponda, kama vyombo vya mfinyanzi utawavunja. 10Sasa nyie wafalme, pambanukeni! Nanyi waamuzi wa nchi, onyekani! 11Mtumikieni Bwana kwa kumwogopa! Mshangilieni kwa kutetemeka! 12Mnoneeni Mwana, asiwatolee makali, mkaangamia njiani! Maana moto wa makali yake utawaka upesi. Wenye shangwe ndio wote wamwegemeao!

