Zekaria 2 (Swahili SRB 37)
1Nilipoyainua macho yangu, nichungulie, mara nikaona mtu, naye alishika mkononi mwake kamba ya kupimia. 2Nikamwuliza: Unakwenda wapi? Akaniambia: Ninakwenda kuupima Yerusalemu, nione, upana wake na urefu wake ulivyo. 3Mara malaika aliyesema na mimi akatoka, kisha malaika mwingine akatokea kukutana naye, 4akamwambia: Piga mbio, umwambie yule kijana kwamba: Yerusalemu utakaa watu pasipo boma kwa wingi wa watu na nyama watakaokuwamo mwake. 5Kisha mimi nitakuwa boma la moto litakalouzunguka nao utukufu wake uliomo mwake utakuwa mimi; ndivyo, asemavyo Bwana. 6Ndivyo, asemavyo Bwana: Haya! Haya! Kimbieni, mwitoke nchi hiyo ya kaskazini! Kwani nimewatawanya ninyi katika pande zote nne za upepo wa angani; ndivyo, asemavyo Bwana. 7Haya! Jiponye, Sioni ukaaye kwake binti Babeli! 8Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kuutokeza utukufu amenituma kwa wamizimu walioziteka mali zenu ninyi, kwani anayewagusa ninyi huigusa mboni ya jicho lake. 9Ndipo, mtakaponiona, nikiwapungia kwa mkono wangu; ndipo, wao watakapokuwa mateka yao walio watumwa wao, mpate kujua, ya kuwa Bwana Mwenye vikosi amenituma. 10Shangilia kwa furaha, binti Sioni! Kwani utaniona, nikija kukaa katikati yako; ndivyo, asemavyo Bwana. 11Siku hiyo itakuwa, wamizimu wengi waje kuandamana na Bwana; ndipo, wao nao watakapokuwa ukoo wangu. Nitakaa katikati yako, upate kujua, ya kuwa Bwana Mwenye vikosi amenituma kwako. 12Ndipo, Bwana atakapowatwaa Wayuda, wawe fungu lake katika nchi hii takatifu, nao Yerusalemu atauchagua tena, uwe mji wake. 13Wote wenye miili ya kimtu sharti wanyamaze kimya usoni pake Bwana, kwani amekwisha kuondoka katika Kao lake takatifu!

