Loguj się
Warumi 10
SRB37

Warumi 10 (Swahili SRB 37)

1*Ndugu, moyo wangu unayapenda sana, ninayomwomba Mungu kwamba: Waisiraeli waokoke. 2Kwani nawashuhudia, ya kuwa waona wivu kwa ajili yake Mungu, lakini hawamtambui. 3Kwani wongofu, Mungu anaoutaka, hawaujui, wakajaribu kujiongoza wenyewe, lakini hivyo hawakuutii ule wongofu, Mungu anaoutaka. 4Kwani timilizo la Maonyo ni Kristo, kila mwenye kumtegemea ajipatie wongofu! 5Kwani Mose aliandika: Anayeufanya wongofu ulioagizwa na Maonyo mtu huyo atapata uzima kwa njia hiyo. 6Lakini wongofu unaopatikana kwa kumtegemea Mungu unasema hivyo: Usiseme moyoni mwako: Yuko nani atakayepaa kwenda mbinguni? Huko ndiko kumshusha Kristo. 7Wala usiseme: Yuko nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? Huko ndiko kumpaza Kristo na kumtoa kwenye wafu. 8Tena unasema: Neno hilo linakukalia karibu, limo kinywani mwako, namo moyoni mwako. Hilo ndilo neno la kumtegemea Mungu, ni hilihili, tunalolitangaza. 9Kwani ukiungama kwa kinywa chako kwamba: BWANA NI YESU, ukamtegemea kwa moyo wako kwamba: Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. 10Kwani ukimtegemea kwa moyo unapata wongofu; ukimwungama kwa kinywa unaokoka. 11Kwani Maandiko yasema: Kila anayemtegemea hatatwezeka. 12Kwani hapa hawachaguliwi Wayuda na Wagriki; kwani aliye Bwana wao wote ni yuyu huyu mmoja, ni mwenye magawio yanayowatoshea wote wanaomtambikia. 13Kwani; Kila atakayelitambikia Jina la Bwana ataokoka. 14Basi, watamtambikiaje, wasiyemtegemea? Tena watamtegemeaje, ambaye hawajamsikia Neno lake? Tena watasikiaje, pasipokuwapo mwenye kutangaza? 15Tena watatangazaje, wasipotumwa? Ndivyo ilivyoandikwa: Tazameni, miguu yao wapiga mbiu njema jinsi inavyopendeza!* 16Lakini walioutii huo Utume mwema sio wote. Kwani Yesaya anasema: Bwana, yuko nani anayeutegemea utume wetu? 17Basi, kumtegemea Mungu huletwa na matangazo, lakini matangazo hutoka katika Neno la Kristo. 18Lakini niseme: Hawakusikia? Kusikia wamesikia. Uvumi wao ulitokea katika nchi zote; nayo maneno yao yalifika hata mapeoni kwa ulimwengu. 19Au niseme: Waisiraeli hawakulitambua? Kwanza Mose anasema: Mimi na niwachokoze ninyi nikiwaletea watu wasio watu, na niwakasirishe ninyi nikiwaletea taifa la watu wasiojua maana. 20Kisha Yesaya anajipa moyo wa kusema: Nimeonwa nao wasionitafuta, nikawatokea wasioniuliza. 21Lakini Waisiraeli anawaambia: Mchana kutwa naliikunjua mikono yangu, nipungie ukoo wa watu wasioonyeka, walio wabishi tu.